Nilikuwa na umri wa miaka 14
nikiwa kwenye jumba la michezo,
nikiiba kwenye mashine ya mchezo,
na nilipokuwa nikitoka nje ya jengo
mlinzi alikamata mkono wangu,
hivyo nikakimbia.
Nilikimbilia mtaani,
na nikaruka juu ya uzio.
Na nilipofika juu,
uzito wa sarafu 3,000 kwenye mkoba wangu
ulinielemea na kunivuta chini.
Niliponyanyuka, mlinzi
alikuwa amesima juu yangu,
na akasema, "Siku nyingine nyinyi vibaka,
ibeni vitu mnavyoweza kubeba."
(Kicheko)
Nilipelekwa kwenye mahabusu ya watoto
na nilipoachiliwa
chini ya dhamana ya mama yangu,
maneno ya kwanza mjomba wangu
alisema yalikuwa, "Ulikamatwaje?"
Nikasema, "Mzee, mkoba
ulikuwa mzito sana."
Akasema, "Mzee,
hukutakiwa kuchukua sarafu zote."
Nikasema, "Mzee, zilikuwa ndogo.
Ningefanyaje?"
na dakika 10 baadaye, alinipeleka kuiba
kwenye mashine nyingine ya mchezo.
Tulihitaji pesa ya petroli kufika maskani.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu.
Nimekulia Oakland, Kalifornia,
na mama yangu
na ndugu wa karibu wa familia
walevi wa madawa ya kulevya ya kokeini .
Mazingira yangu yalijumuisha
kuishi na familia, marafiki,
na makazi kwa wasio-na-makazi.
Mara nyingi, mlo wa jioni tuliupata
kwenye foleni za vyakula vya msaada.
Mjomba aliniambia hivi:
pesa inatawala dunia
na kila kitu ndani yake.
Na katika hii mitaa, pesa ni Mfalme.
Na ikiwa utafuata pesa,
itakupeleka kwa mtu mbaya au mtu mzuri.
Baadaye kidogo,
nilifanya uhalifu wangu wa kwanza,
na ndiyo mara ya kwanza
nilipoambiwa kuwa nina kipaji
na nikajisikia kuwa kuna mtu ananiaminia.
Hakuna aliyewahi-niambia kuwa
ningeweza kuwa mwanasheria,
daktari au mhandisi.
Yaani, ningewezaje kufanya hivyo?
Sikuweza kusoma, kuandika wala kutahajia.
Sikuwa mtu aliyesoma.
Kwahiyo, mara zote nilifikiri
uhalifu ndio njia ya kwenda.
Na kisha siku moja
Nilikuwa naongea na mtu
na alikuwa ananiambia juu ya
huu wizi ambao tungeweza fanya.
Na tukaufanya.
Ukweli ni kwamba nilikuwa nakulia
kwenye nchi yenye uwezo mkubwa
wa kifedha duniani,
Marekani,
huku nikiangalia mama yangu,
akisimama kwenye foleni ya benki ya damu
kuuza damu yake kwa Dola 40
kujaribu tu kulisha wanae.
Bado ana alama za sindano
mikononi mwake leo kudhihirisha hilo.
Kwa hiyo sikuijali jumuiya yangu,
Hawakujali maisha yangu.
Kila mtu pale alifanya anachotaka fanya kupata alichotaka,
wauza mihadarati,
wezi, benki ya damu.
Kila mtu alichukua fedha ya damu.
Hivyo nilipata yangu
kwa njia yoyote ile.
Nilipata yangu.
Elimu ya fedha
kweli ilitawala dunia,
na nilikuwa mtoto mtumwa kwake
nikifuata mtu mbaya.
Nikiwa na miaka 17,
nilikamatwa kwa wizi na mauaji
na punde nikajifunza kuwa fedha jela
zinatawala zaidi ya zilivyo mitaani,
Hivyo nilitaka kuingia.
Siku moja, nilikurupuka kushika
ukurasa wa michezo katika gazeti
ili mfungwa mwenzangu anisomee,
na kwa bahati mbaya
nikachukua sehemu ya biashara.
Na huyu mzee akasema,
"Hey, kijana, umechukua hisa?"
Na nikasema, "Ndio nini hicho?"
Akasema, "Hiyo ndiyo sehemu ambayo
watu weupe huweka pesa yao yote."
(Kicheko)
Na ilikuwa ndiyo mara ya kwanza
nilipata ono fupi la tumaini,
siku za baadaye.
Alinipa maelezo mafupi
ya hisa zilikuwa ni nini,
lakini ilikuwa ni muhtasari tu.
Yaani, ningewezaje kuifanya?
Sikuweza kusoma, kuandika wala kutahajia.
Ujuzi niliokuwa nimeukuza
kuficha kutokusoma kwangu
haukufanya kazi tena
katika mazingira haya.
Nilikuwa nimenaswa kwenye kizimba
mateka kati ya watekaji,
nikipigania uhuru ambao sijawahi kuwa nao.
Nilikuwa nimepotea, nimechoka,
na sikuwa na machaguzi.
Kwa hiyo nikiwa na miaka 20,
nilifanya kitu kigumu kuliko vyote
nilivyowahi kufanya maishani mwangu.
Nilichukua kitabu,
na ilikuwa ni kipindi kigumu sana
maishani mwangu.
kujaribu kujifunza jinsi ya kusoma,
kutengana na familia yangu,
na rafiki zangu.
Ilikuwa shida, mzee.
Ilikuwa ni mahangaiko.
Lakini sikufahamu japo kidogo kuwa
nilikuwa napata zawadi kubwa kuliko zote
nilizowahi kuziota,
kujithamini,
maarifa, nidhamu.
Nilisisimka mno kusoma, kiasi kwamba
nilisoma kila kitu nilichokitia mkononi:
makaratasi ya pipi, nembo za nguo,
alama za barabarani, kila kitu.
Nilikuwa nikisoma tu vitu!
(Makofi na Vifijo)
kusoma tu vitu.
Nilisisimka sana kujua jinsi ya kusoma
na kujua jinsi ya kutahajia.
Rafiki alikuja, akaniuliza,
"Mzee, unakula nini?"
Nikasema, "P-I-P-I, pipi."
(Kicheko)
Akasema, "Nipe kidogo."
Nikasema, "L-A. La."
(Kicheko)
Ilikuwa babukubwa.
Yaani, sasa naweza, kwa mara ya kwanza
katika maisha yangu, kusoma.
Hisia niliyoipata, ni ya kustaajabu sana.
Kisha, nikiwa na miaka 22,
nikijisikia mwenyewe,
nikijiamini,
Nilikumbuka kile yule mzee aliniambia.
Kwa hiyo nilichukua
kurasa za biashara za gazeti.
Nilitaka kuwatafuta hawa matajiri weupe.
(Kicheko)
Kwa hiyo nilitafuta ule muhtasari.
Nilipokuwa nikijiendeleza kikazi
nikifundisha wengine namna ya
kusimamia fedha na kuwekeza,
punde nikajifunza kuwa
nilihitaji kuwajibika kwa matendo yangu.
Kweli,
nilikulia kwenye mazingira tata sana,
lakini nilichagua kufanya uhalifu,
na nilipaswa kukiri hilo.
Nilipaswa kuwajibika kwa hilo,
na nilifanya hivyo.
Nilikuwa nikiunda mtaala ambao
ungeweza kuwafundisha wafungwa
namna ya kusimamia fedha
kupitia ajira za gerezani.
Kutiisha mtindo wetu wa maisha
kungeweza kutoa zana zihamishikazo
ambazo tunaweza kuzitumia kusimamia fedha
tunapoirudi kwenye jamii,
kama watu wengi walivyofanya
ambao hawakufanya uhalifu.
Kisha niligundua
kulingana takwimu ya MarketWatch,
zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa Marekani
wana chini ya Dola 1,000 katika akiba.
Michezo ilielezea kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wachezaji wa NBA
na wachezaji wa NFL hufilisika.
Asilimia 40 ya matatizo ya ndoa
hutokana na masuala ya kifedha.
Balaa gani?
(Kicheko)
Unataka kuniambia,
watu wamefanya kazi maisha yao yote,
wakinunua magari, nguo, nyumba
na vitu mbalimbali
lakini walikuwa waliishi hundi kwa hundi?
Ni namna gani duniani wanajamii
wangekwenda kuwasaidia wafungwa
kurudi kwenye jamii
ikiwa hawakuweza kusimamia
mambo yao wenyewe?
Tumevurugwa.
(Kicheko)
Nahitaji mpango mzuri zaidi.
Hii haitakwenda kufanya kazi vizuri.
Hivyo ...
Nilifikiria.
Sasa nilikuwa na wajibu kukutana
na wale waliokuwa kwenye mkondo huo
na kuwasaidia,
na ilikuwa ni ajabu sababu
sasa nilijali jumuiya yangu
Lo, hebu fikiria.
Nilijali kuhusu jumuiya yangu.
Ujinga juu ya Fedha ni ugonjwa
ambao umedhohofisha wachache
na walio chini katika jamii yetu
kwa vizazi na vizazi,
na tunapaswa kukasirika juu ya hilo.
Ebu jiulize:
Inawezekanaje asilimia 50
ya wakazi wa Marekani
wasiwe na elimu ya fedha katika nchi
inayoendeshwa kwa ustawi wa kifedha?
Kupatikana kwa haki kwetu,
hadhi yetu ya kijamii,
hali ya maisha, usafirishaji na chakula
vyote vinategemea fedha
ambayo watu wengi hawawezi kuisimamia.
Ni ajabu!
Ni janga
na hatari kubwa kwa usalama wa umma
kuliko suala jingine lolote.
Kadiri ya
Kitengo cha Urekebishaji cha Kalifornia,
zaidi ya asilimia 70 ya wale waliofungwa
wamefanya au wameshtakiwa kwa uhalifu
uhusianao na fedha:
wizi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba,
kutapeli, uporaji, ghusubu --
na orodha inaendelea.
Angalia hii:
Mfungwa wa kawaida
huingia katika mfumo wa gereza
wa Kalifornia
pasipo kuwa na elimu ya fedha,
hupata ujira wa senti 30 kwa saa,
zaidi ya Dola 800 kwa mwaka,
bila ya kuwa na matumizi yoyote
na kuweka akiba yoyote.
Anapopewa msamaha,
hupewa dola 200 pesa ya geti na kuambiwa,
"Wee, mafanikio mema, kaa mbali na
matatizo. Usirudi gerezani tena."
Bila kuwa na maandalizi yoyote ya maana
au mpango fedha wa muda mrefu,
anafanyaje ...?
Akiwa na miaka 60?
Apate kazi nzuri,
au arudi kwenye tabia ile ile ya uhalifu
iliyompeleka gerezani kwanza?
Nyinyi walipakodi, chagueni wenyewe.
Hakika, elimu yake
imeshamchagulia, pengine.
Kwa hiyo, tunatibuje ugonjwa huu?
Nilishiriki kuanzisha programu
tuliyoiita Elimu Hisia
ya Uwezeshaji wa Kifedha
tunaiita FEEL
na inafundisha namna ya kutenganisha
maamuzi ya kihisia
na maamuzi ya kifedha,
na sheria 4 aushi
za utawala fedha binafsi:
njia sahihi ya kuweka akiba,
kudhibiti gharama zako za maisha,
kukopa fedha kwenye ufanisi
kutawanya fedha yako
kuruhusu fedha yako ikufanyie kazi
badala ya wewe kuifanyia kazi.
Wafungwa wanahitaji ujuzi huu
kabla ya kuingia tena kwenye jamii.
Hatuwezi kubadilika kuwa na maisha
ya kawaida bila ujuzi huu wa maisha.
Hii dhana kuwa ni Weledi tu
wanaweza kuwekeza na kusimamia fedha
ni ya fedheha kabisa,
na yeyote aliyewaambia hivyo anadanganya.
(Makofi na Vifijo)
Mweledi ni mtu
anayejua kazi zake kuliko walio wengi,
na hakuna mtu ajuaye kiasi gani cha fedha
wahitaji, unacho, au wataka zaidi ya wewe,
ikimaanisha kuwa wewe ni mweledi.
Elimu ya fedha siyo stadi,
mabibi na mabwana.
Ni mtindo wa maisha.
Uimara wa kifedha ni matokeo ya ziada
ya mtindo sahihi wa maisha.
Mfungwa mwenye elimu nzuri ya kifedha
anaweza kuwa mwananchi mlipakodi,
na mwananchi mlipakodi mwenye elimu
nzuri ya kifedha anaweza kubaki hivyo.
Hii inatuwezesha kuunda daraja
kati ya wale watu tunaowashawishi:
familia, marafiki na wale vijana
ambao bado wanaamini
kuwa uhalifu na pesa vina uhusiano.
Kwa hiyo tupoteze uwoga na wasiwasi
wa maneno makubwa ya kifedha
na ujinga mwingine wote
ambao mmekuwa mkisikia huko nje.
Na tujikite kwenye kiini
kilichokuwa kinadhoofisha jamii yetu
kuanzia kutimiza wajibu wako
la kuwa meneja mzuri wa maisha.
Na tutoe mtaala mwepesi na rahisi kutumia
ambao utaingia kwenye kiini, kiini
cha ni nini ukweli wa
uwezeshaji wa kifedha na elimu ya hisia.
Sasa, ikiwa umekaa hapa kwa wasikilizaji
na umesema,
"Ndiyo, kweli, hiyo si mimi
na sikubaliani nayo,"
basi njoo uchukue somo langu --
(Kicheko)
ili nikuoneshe ni kiasi gani cha pesa
inakugharimu kila unaposhikwa na hisia.
(Makofi na Vifijo)
Asanteni sana. Asanteni.
(Makofi na Vifijo)