Njiani kufika hapa, nilikuwa na mazungumzo mazuri na mtu aliyekuwa anakaa pembeni yangu kwenye ndege. Alinambia "Hamna kazi tena USA, yaani sasa wamebuni kazi mpya: mwanasaikolojia wa paka, mzungumzaji wa mbwa,msasi wa kimbunga." Punde, aliniuliza, "Kwani wewe unafanya kazi gani?" Nikamjibu, "Mjenzi wa usalama?" (Vicheko) Kila siku, nafanya bidii kuwazidishia wanawake sauti na kuoneysha maisha yao na michango yao katika hatua za kutafuta usalama na kutatua migogoro, na kwa sababu ya kazi zangu, natambua kwamba njia ya pekee kwa kuhakikisha ushirikiano kamili wa wanawake duniani ni kuchukua tena dini mikononi mwetu. Sasa, jambo hilo ni muhimu sana kwangu. Kama muislamu na mwanamke kijana, ninaijali dini yangu sana. Inanipa nguvu na msimamo katika kazi zangu kila siku. Ndiyo sababu inayoniwezesha kusimama hapa leo mbele yenu. Lakini siwezi kutojali hasara kubwa zilizofanyika kwa kutumia jina la dini, si dini yangu tu, lakini dini zote kubwa za dunia. Kuyatumia vibaya na kuyageuza maandiko ya kidini kumebadilisha desturi zetu za kijamii na kitamaduni, sheria zetu, kila siku zetu, hadi kumefikia tusipoweza kupagundua. Wazazi wangu walihama Libya, Afrika ya Kaskazini kwenda Kanada mwanzoni mwa miaka 1980, na mimi niko katikati ya watoto 11. Ehee, 11. Lakini katika kukulia kwangu, niliwaona wazazi wangu, wote wacha Mungu na waumini wa Akhera, wakisali na kumshukuru kwa baraka zao, kama mimi, lakini zinginezo pia. (Vicheko) Walikuwa na huruma, wenye kuchekesha, na wenye subira, subira kubwa, aina inayofunzwa kwa kuwalea watoto 11. Pia walifanya haki. Sikuwahi kupaswa kuijua dini kwa mtazamo wa kitamaduni tu. Nilitendewa sawasawa na kaka zangu, na sisi sote tulikuwa tunatarijiwa kufanya sawasawa. Sikuwahi kuambiwa kwamba Mungu huhukumu tofauti kwa jinsia. Wazazi wangu walimwona Mungu kuwa Mwingi wa Rehema, Fadhila na rizki na mimi nilichukulia msimamo wao. Kwa uhakika, malezi yangu yalikuwa na faida zake. kuwa katikati ya watoto 11 ni kama Diplomasia 101. (Vicheko) Mpaka leo, watu huniuliza wapi nilipokwenda skule, kama, “Ulienda Skule ya Kennedy ya Serikali?" na mimi huwatazama na kuwambia, “Hapana, Nimeenda Skule ya Murabit ya Mambo ya Kimataifa.” Ni maalum sana. Ungeongea na Mamangu kwa kujipatia nafasi Lakini kwa bahati yenu, yupo leo. Lakini kuwa miongoni wa watoto 11, na kuwa na ndugu 10, kunafundisha mengi kama mifumo ya mamlaka na muungano. Kama kuzingatia lengo; useme haraka au usiseme sana, kwa sababu utadakiwa mazungumzo kila mara. Kunafundisha umuhimu wa kuwa mjumbe mzuri. Uyaulize maswali kwa mpango kwa kupata jibu unalolitaka, na ujue kusema 'la' kwa mpango pia kwa kufuliza usalama. Lakini funzo muhimu sana nililolipata kutoka utoto wangu lilikuwa umuhimu wa kuwa na nafasi kwenye meza. Taa yake ndogo mamangu ilipovunjika, alivyoipenda sana, ilinilazimu niwepo wakati alipochunguza ilikuwaje, ili nijitetee, kwa sababu kama hupo, lawama inakuangukia kwako, na kabla hujagundua, utakuwa umeadhibiwa. Kwa uhahika, sijapewa adhabu mimi mwenyewe. Nilipokuwa na miaka 15 mwakani 2005, nikatimiza skule ya sekondari nikahamia Kanada-- Saskatoon -- Ila Zawiya, Libya, mji wa nyumbani wa wazazi wangu, mji wa kidesturi sana. Fikiri, muda huo niliwahi kufika Libya kwa ajili ya matembezi tu, na kama msichana wa miaka 7, ilipendeza sana. Ilikuwa aiskrimu na pwani na jamaa wenye furaha. niligundua haiko vilevile kama msichana wa miaka 15. Nikakutana upesi na mambo ya dini ya kiutamaduni. Maneno ya "haramu" -- lenye maana ya kukatazwa kidini -- na "aibu" -- lenye maana ya kutofaa kimaadili -- yalibadilishanwa bila mpango. kama yalikuwa na maana moja na adhabu moja vilevile. Nikajikuta sana katika mazungumzo na wenzangu wa skule na wa kazi, profesa, rafiki zangu na hata jamaa zangu, nikaanza kujiuliza kuhusu desturi zangu na malengo yangu. Na hata na msingi mzuri niliopokea kutoka wazazi wangu, Nilijikuta nikajiuliza kuhusu nafasi ya mwanamke katika dini yangu. Kule kwenye Skule ya Murabit ya Mambo ya Kimataifa, tunapenda sana kufanya mjadala, na sheria ya kwanza ni fanya utafiti wako, na hivyo ndivyo nilivyofanya mimi, Ikanishangaza sana vipi ilikuwa rahisi kuwagundua wanawake katika Uislamu waliokuwa viongozi, wavumbuzi, wenye nguvu -- za kisiasa, za kiuchumi hata za kijeshi. Khadija aliziendesha fedha za harakati za Kiislamu katika siku zake za mwanzo. Tusingekuwepo hapa leo bila michango yake. Kwa nini tusifundishwe kisa chake? Kwa nini tusifundishwe visa vya hao wanawake? Kwa nini wanawake wapewe vyeo vilivyotoka zama zilizotangulia mafunzo ya dini yetu? Na kwa nini, kama sisi sote tuko sawasawa machoni mwa Mungu, hatuko sawasawa machoni mwa binadamu? Hayo yalinipeleka kufikiria mafunzo yangu ya utotoni. Anayeamua, na kuwa na mamlaka juu ya ujumbe, anayo nafasi kwenye meza, na kwa bahati mbaya, katika dini zote za kidunia, hao si wanawake. Taasisi za kidini zinatawaliwa na wanaume na kuendeshwa na viongozi vya kiume, na wanabuni sera zinazowafaa wanaume tu, na ila tunaweza kubadilisha mfumo huo kabisa, kwa kweli hatuwezi kutarajia wanawake kushiriki kwa ukamilifu katika uchumi au siasa. Msingi wetu umevunjika. Mamangu husema, "huwezi kujenga nyumba nzima juu ya msingi mbovu". Mwakani 2011, Mapinduzi ya Libya yaliripuka na aila yangu walikuwepo mistari ya mbele. Kuna jambo moja la kushangaza linalojitokeza katika vita, kama mageuzo ya kiutamaduni, kwa muda mfupi tu. Kwa mara ya kwanza nilijisikia ilikubaliwa, au hata ilisisitizwa kwa mimi kujihusisha na mambo. Ilihitajika. Mimi na wanawake wengine walipewa nafasi kwenye meza. Hatukuwa wasaidizi wa wanaume tu. Tulichangia katika uamuzi. Tulichangia katika kutoa taarifa. Tulikuwa muhimu sana. Na mimi nilitaka, nilihitaji mageuzo hayo kutoondoka. Lakini niligundua si rahisi kuwa nilivyotaka. Ilichukua wiki chache tu kabla hao wanawake niliowafanya nao kazi walikuwa wanarejea katika kazi zao za zamani, na wengi walipewa maneno ya kusisitizwa kutoka kwa viongozi wa kidini na vya kisiasa, wengi wao walijaribu kuthibitisha hoja zao kwa maandishi ya kidini. Ndivyo walivyojipatia mikono ya watu katika hoja zao. Mwanzoni, nilizingatia kuwapa wanawake nguvu katika siasa na uchumi. Nikafikiri ingeliongoza mabadiliko ya kiutamaduni na kijamii. Niligundua, ilifanikiwa kidogo tu, lakini sio sana. Nikaamua kuitumia njia yao wale viongozi wa kidini nikaanza kuthibitisha hoja zangu kwa maandishi ya kiislamu pia. Katika miaka 2012 na 2013, shirika langu liliongoza kampeni ya pekee iliyokuwa kubwa na pana kuliko zote Libya. Tulipenyeza nyumbani, skuleni na vyuoni, hata misikitni. Tulizungumza na watu 50,000 uso kwa uso, na mamia ya maelfu zaidi kwa njia za matangazo ya kubandika, matangazo kwenye tv na kwenye radio. Labda mnajiuliza, shirika la haki za wanawake waliweza kufanya hivyo vipi katika jamii ilyopingana na sisi kabisa mwanzoni. Niliyatumia maandishi ya kiislamu. Nilitumia aya za Korani na misemo ya Mtume Mohammed, Hadithi zake, misemo yake ambayo ni, kwa mfano, "Mtu bora ndiye anayefanya wema kwa familia yake." "Usimruhusu mtu kumdhulumu mwingine." Kwa mara ya kwanza, hotuba za Ijumaa kutoka kwa imamu wa kienyeji zilitangaza haki za wanawake. zilizungumzia masuala yasiyo kawaida, kama vurugu ya nyumbani. Sera zilibadilishwa. Katika jamii fulani, ilitubidi kusema lile Azimio la Kimataifa la Haki ya Wanadamu mlilopingana nayo kwa sababu haikuandikwi na watalaamu wa kidini, eti, misingi yote ile imo kitabu chetu. Yaani, Shirika la Umoja wa Mataifa lilituiga tu. Kwa kuubadilisha ujumbe wenyewe, tuliweza kuitoa sura mpya iliyotangaza haki za wanawake Libya. Ni jambo ambalo sasa limeigwa duniani, na sisemi ni rahisi--- niamini, si rahisi kabisa. 'Liberals' watasema unaitumia dini na kukuita 'conservative' mbaya. na 'conservatives' watakupa matusi mengi. Mimi mwenyewe nimeyapata mengi, kama "Wazazi wako hawaaibiki na wewe?" -- sio kweli; wao wananipenda kuliko wote -- au "Hutoishi kuona siku yako ya kuzaliwa tena" -- tena sio kweli, nimeshaiona. Na bado, ninaamini kabisa kwamba haki za wanawake na dini zinaweza kuendana. Lakini lazima tupewe nafasi kwenye meza. Tusiache kupigania nafasi yetu, kwa sababu kwa kukaa kimya, tunaruhusu mateso na dhuluma za wanawake duniani kuendelea. Kwa kudai tutapigania haki za wanawake na kupigania ugaidi kwa kutumia mabomu na vita, tunaharibu jamii za kienyeji zinazohitaji kuyashughulikia masuala hayo ili yawezekane kuendelea. Sio rahisi, kushindana na taarifa za dini za kupotosha. Utapata vyako vya matusi na dhihaka na vitisho. Lakini ni lazima ifanyike. Hatuna budi ila kuuchukua tena ujumbe wa haki za binadamu, maadili ya dini yetu, si kwa ajili yetu, na si kwa ajili ya wanawake wenu tu, si kwa ajili ya wanawake humu leo, hata si kwa ajili ya wanawake kule nje, bali kwa ajili ya jamii ambazo zingebadilika kuwa nzuri kwa mashirikiano ya wanawake. Na jinsi ya pekee sisi tunavyoweza kufanya hivyo, njia yetu moja tu, ni kupata nafasi na kukaa daima, kwenye meza. Asante. (Makofi)