Leo niko hapa kuongea kuhusu swala nyeti, ambalo lina jibu tatanishi. Swala langu ni zile siri za ugomvi nyumbani, na swali nitakalokabiliana nalo ni lile swali moja kila mmoja huliuliza kila mara: Kwa nini muathirika hubakia? Kwa nini mtu yeyote abaki na mume ampigaye? Mie si daktari wa akili, mfanyakazi wa ustawi wa jamii au mtaalam wa ugomvi wa nyumbani. Mimi ni mwanamke mwenye hadithi ya kusimulia. Nilikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili. Nilikuwa nimehitimu tu kutoka chuo cha Harvard. Nilikuwa nimehamia mjini New York kwa ajili ya kazi yangu ya kwanza kama mwandishi na mhariri wa gazeti la Seventeen. Nilikuwa na nyumba yangu ya kwanza, kadi yangu ya kwanza ya American Express, na nilikuwa na siri moja kubwa sana. Siri yangu ilikuwa kwamba kulikuwa na bunduki iliyojaa risasi iliyoelekezwa kichwani mwangu na mwanamme niliyefikiria alikuwa mpenzi wangu, mara kadhaa. Mwanamme huyu niliyempenda kuliko yeyote duniani alielekeza bunduki kichwani mwangu na kutishia kuniua mara nyingi kuliko zile ningeweza kukumbuka. Niko hapa kuwapa hadithi ya upendo wa kupindukia, mtego wa kisaikolojia uliofichwa kama mapenzi, ambao mamilioni ya wanawake na hata wanaume wengine hutumbukia kila mwaka. Inaweza hata kuwa hadithi yako. Sionekani kama mtu niliyenusurika na ugomvi katika mahusiano. Nina shahada ya sanaa katika Kiigereza kutoka chuo cha Harvard, na shahada ya juu katika mauzo kutoka kwa chuo cha biashara cha Wharton. Nimetumia muda mrefu maishani nikifanya kazi kwenye kampuni bora duniani zikiwemo Johnson & Johnson, Leo Burnett na The Washington Post. Nimeolewa takriban miaka ishirini kwa mme wangu wa pili na tuna wana watatu pamoja Mbwa wangu ni mweusi, na mie huendesha gari ndogo la Honda Odyssey. (Kicheko) Kwa hivyo ujumbe wangu wa kwanza kwenu ni kwamba ugomvi wa nyumbani humtokea yeyote-- kila jamii,dini, kila kipato na ngazi ya kimasomo. Iko kila mahali. Na ujumbe wangu wa pili ni kwamba kila mtu hufikiri ugomvi wa nyumbani huwaathiri wanawake, ati ni swala la wanawake. Si sahihi. Zaidi ya asili mia 85 ya wanyanyasaji ni wanaume, na ugomvi wa nyumbani hutokea haswa katika mahusiano ya undani, ya kutegemeana na yale ya muda mrefu, yaani, katika familia, mahali tusipotaka au kutarajia kupata ugomvi, ndio sababu tuhuma za kinyumbani ni tatanishi hivi. Ningekuambia kwamba ningekuwa mtu wa mwisho duniani kukaa na mwanaume anayenipiga, lakini kusema kweli nilikuwa mwathirika kwa sababu ya umri wangu. Nilikuwa mwenye umri wa miaka ishirini na mbili na Marekani, wanawake wenye umri kati ya miaka kumi na sita hadi ishirini na nne wana uwezekano wa mara tatu zaidi kuwa waathirika wa ugomvi wa nyumbani ikilinganishwa na wanawake wa umri mwingine, vilevile zaidi ya wanawake mia tano na wasichana wa umri huu huuawa kila mwaka na wapenzi wanyanyasaji, wapenzi, na waume zao Marekani. Nilikuwa muathirika kwa sababu sikujua chochote kuhusu ugomvi wa nyumbani, maonyo yake ama mifano yake. Nilikutana na Conor usiku mmoja wenye baridi na mvua, mwezi wa Januari. Alikaa kando yangu kwenye treni katika mji wa New York, na alianza kuniongelesha. Aliniambia mambo mawili. La kwanza kuwa, yeye pia, alikuwa amehitimu kutoka kwa kati ya zile shule bora zaidi Marekani, na kwamba alifanya kazi kwenye benki moja ya kuvutia sana huko Wall Street. Lakini kile kilichonivutia zaidi siku hiyo ni kuwa alikuwa mwerevu na mcheshi na alionekana kuwa kijana wa mashambani. Alikuwa na haya mashavu makubwa, haya mashavu makubwa ya waridi na hii nywele za rangi kama ya ngano, na alionekana kuwa mwema sana. Jambo moja la busara Conor alilofanya, kutoka mwanzoni, lilikuwa kufanya kana kwamba nilikuwa mwenye ushawishi mkubwa katika huo uhusiano. Alifanya hivi haswa hapo mwanzo kwa kunihusudu. Tukaanza kutoka pamoja, na alipenda kila kitu kunihusu, ati nilikuwa mwerevu, ati nilisomea chuo cha Harvard, ati nilikuwa mwenye shauku kusaidia wasichana wadogo, na kazi yangu. Alitaka kujua kila kitu kuhusu familia yangu na utoto wangu na matarajio na ndoto zangu. Conor alikuwa na imani nami, kama mwandishi na mwanamke, kwa njia ambayo yeyote mwengine alikuwa hajawahi. Na alileta uaminifu kati yetu kwa kunieleza siri yake, ambayo ilikuwa, alipokuwa mvulana mdogo sana akiwa na umri wa miaka minne alipigwa vibaya sana mara kwa mara na babake wa kambo, na unyanyasaji ulizidi kuwa mbaya zaidi hadi ikambidi aache shule akiwa daraja la nane, ingawa alikuwa mwerevu sana, na kwamba alitumia takriban miaka ishirini kujenga maisha yake upya. Ndiyo sababu hiyo shahada yake kutoka zile shule bora zaidi Marekani, na kazi yake Wall Street na maisha yake mazuri siku za usoni zilikuwa za umuhimu mkubwa sana kwake. Kama ungeniuliza kama huyu mwanamme mwerevu, mcheshi na mwenye kujali aliyenipenda sana angekuja kuniamulia kama ningejipamba au la, ufupi wa sketi zangu, mahali ningeishi, kazi gani ningefanya, marafiki zangu wangekuwa wepi na pale ningekulia Krisimasi ningekucheka, kwa sababu hakukuwa na ushahidi wowote wa tuhuma au uthibiti au hasira kutoka kwa Conor hapo mwanzoni. Sikujua kwamba daraja la kwanza katika uhusiano wowote wenye ugomvi ni kumvuta na kumpumbaza mwathirika Pia sikujua kuwa daraja ya pili ni kumtenga mwathirika. Conor hakuja nyumbani siku moja na kutangaza, "Unajua huu uhusiano wetu kama wa Romeo na Julieti umekuwa mtamu, lakini nataka kwenda katika hatua inayofuata ambapo nitakutenga na kukunyanyasa" - (Kicheko) - "kwa hivyo nataka kukuhamisha kutoka nyumba hii ambapo majirani wanawezakusikia ukipiga mayowe na kukupeleka nje ya mji huu ambapo una marafiki na familia na wafanyakazi wenzako wanaoweza kuona hiyo michubuko." Badala yake, Conor alikuja nyumbani jioni ya Ijumaa moja na akaniambia kuwa alikuwa ameacha kazi siku hiyo, kazi ya ndoto zake, na akasema kwamba alikuwa ameacha kazi hiyo kwa sababu yangu, kwa sababu nilimfanya ahisi usalama na kupendwa ati hakuhitaji tena kujithibitisha huko Wall Street, na alitaka tu kutoka mjini na kukaa mbali na familia yake iliyomnyanyasa. na kuhamia mji mdogo wa New England ambapo angeweza kuanza upya maisha yake nikiwa kando yake. Sikutaka kamwe kuhama kutoka New York, na kuacha kazi ya ndoto zangu, lakini nilifikiria mtu hujitoa muhanga kwa mpenzi wake, kwa hivyo nikakubali na nikaacha kazi yangu, na Conor na mimi tukaondoka Manhattan pamoja. Sikuwai kufikiria kwamba penzi nililokuwa nalo halikuwa la kawaida, na kwamba nilikuwa nikitembea bila habari ndani ya mtego mzuri wa kimwili, kifedha na kiakili Daraja ya pili katika ugomvi wa kimahusiano ni kuleta tishio la vurugu na kuangalia vile linavyomgusa. Na hapa ndipo bunduki zinapoingia. Muda tu tulipohamia New England--unajua, mahali Connor aliposema pangemfanya ajisikie salama-- alinunua bunduki tatu. Aliweka moja garini. Aliweka moja chini ya mto kitandani mwetu, na ya tatu alitembea nayo mfukoni nyakati zote. Na alisema alihitaji bunduki hizo kwa sababu ya uchungu aliopitia akiwa mchanga. Alizihitaji kujisikia salama. Lakini bunduki hizo zilikuwa ujumbe kwangu, na ingawa hakuwai kuninyoshea mkono, maisha yangu tayari yalikuwa hatarini kila dakika ya kila siku. Kwanza Conor alinishambulia siku tano kabla ya harusi yetu. Ilikuwa saa moja asubuhi na bado nilikuwa nimevalia vazi la kulala Nilikuwa nafanya kazi kweny kompyuta yangu nikijaribu kumaliza kazi fulani ya uandishi, na nilikuwa nimekasirika, na Conor akatumia hasira zangu kama kisingizio kunikaba koo na kuikaza hadi sikuweza kupumua au kupiga kelele, na alitumia mkazo huo kugonga kichwa changu mara kadhaa kwenye ukuta. Siku tano baadaye, ile michubuko kumi shingoni mwangu ilipotea na nikavaa nguo ya mama yangu ya harusi, na nikafunga ndoa naye. Licha ya yaliyotokea, nilikuwa na hakika tungeishi maisha ya raha milele, kwa sababu nilimpenda, na alinipenda sana. Na aliniomba msamaha. Alikuwa amechoshwa sana na mipango ya harusi yetu na kwa kuwa kitu kimoja na mimi. Halikuwa jambo la kawaida na asingeniumiza tena. Ilitokea mara mbili katika fungate. Mara ya kwanza, nilikuwa naendesha gari kutafuta ufukwe wa siri na nikapotea, na akanipiga ngumi nzito kwenye upande wa kichwa changu hata ule upande mwengine wa kichwa changu ukagonga dirisha lililo kando ya dereva mara kadhaa. Alafu tena siku chache baadaye, tukielekea nyumbani baada ya likizo ya harusi, alikasirishwa na trafiki, na akarusha Big Mac baridi usoni mwangu. Conor aliendelea kunipiga mara moja au mbili kwa wiki kwa miaka miwili na nusu ya ndoa yetu. Nilifanya makosa kufikiria nilikuwa wa kipekee na peke yangu katika hali hii. Mmoja kati ya wanawake watatu wakiAmerika hupitia ugomvi wa nyumbani ama kufuatwa fuatwa wakati mmoja maishani mwake, na CDC inaripoti kwamba watoto milioni kumi na tano wananyanyaswa kila mwaka, milioni kumi na tano. Hivyo basi, nilikuwa kwenye ushirika mzuri sana. Kurudia swali langu: Kwa nini nilibaki? Jibu lenyewe ni rahisi. Sikujua alikuwa akininyanyasa. Hata ingawa alielekeza bunduki zilizo na risasi kichwani mwangu, akanisukuma ngazini, akatishia kuua mbwa wetu, akatoa ufunguo wa gari nikiendesha barabarani, akamwaga maganda ya kahawa kichwani mwangu nikijitayarisha kwa mahojiano ya kazi, SIkuwai hata mara moja kujihisi kuwa mke anayenyanyaswa. Badala yake, nilikuwa mwanamke mwenye nguvu alimpenda sana mwanaume aliyekuwa na shida, na nilikuwa mtu wa pekee duniani ambaye angeweza kumsaidia Conor kukabiliana na mashetani yake. Swali lingine kila mtu huuliza ni, kwa nini hatoki tu? Kwa nini sikuondoka? Ningeweza kuondoka wakati wowote. Kwangu mimi, hili ndilo swali chungu na la kuhuzunisha zaidi ambalo watu huniuliza, kwa sababu sisi waathiriwa tunajua jambo nyinyi msilojua: Ni jambo la hatari sana kumtoroka mnyanyasaji. Kwa sababu daraja ya mwisho katika tuhuma za kinyumbani ni kumuua. Zaidi ya asilimia sabini ya vifo vinavyosababishwa na tuhuma za kinyumbani hutokea baada ya mwathiriwa kukatiza uhusiano huo, baada ya kutoka, kwa sababu wakati huo mnyanyasaji hana chochote cha kupoteza. Matokeo mengine ni pamoja na kufuatwa fuatwa, hata baada ya mnyanyasaji kuoa tena; unyimaji wa hela; na uingiliaji wa mfumo wa mahakama za kifamilia ili kumtia wasiwasi mwathirika na wanawe, ambao mara kwa mara hushurutishwa na majaji wa mahakama za kifamilia kuwa na wakati usiosimamiwa pamoja na mtu yule aliyemtuhumu mama yao. Na bado twauliza, kwa nini hamtoroki tu? Niliweza kuondoka, kwa sababu ya kipigo kibaya cha mwisho kilichofumbua macho yangu. Nilitambua kwamba mtu yule niliyempenda sana angekuja kuniua kama ningeendelea kumuacha hivi hivi tu. Hivyo nikavunja ukimya. Nikawaeleza watu wote: polisi, jirani zangu, marafiki zangu na familia, wageni, na niko hapa leo kwa sababu nyote mlinisaidia. Tuna tabia ya kuwabagua waathirika kama vichwa vibaya vya habari, wanaojitakia maovu, watu walioharibika. Swali hilo, "Kwa nini haondoki?" kwa wengine ni kama kusema, "Ni makosa yake kuendela kukaa hapo," kana kwamba waathirika huchagua kusudi kupenda wanaume walio na lengo la kutumaliza. Lakini tangu niandike kitabu "Crazy Love," nimesikia mamia ya hadithi kutoka kwa wanaume na wanawake ambao pia waliondoka, waliojifunza somo muhimu la maisha kutokana na yale yaliyotokea, na waliojenga maisha yao tena--maisha yenye furaha kama wafanyakazi, wake na kina mama, maisha yasiyo na unyanyasaji, kama yangu. Kwa sababu inaonekana kwamba mimi nilikuwa mwathirika halisi wa unyanyasaji majumbani. na msalimika wa unyanyasaji wa majumbani. Niliolewa na mtu mwema na mpole, na pamoja tuna watoto watatu. Nina yule mbwa wangu mweusi, na nina lile gari ndogo. Kile sitawahi kuwa nacho tena, milele, ni bunduki iliyojaa risasi iliyoelekezwa kichwani mwangu na mtu anayesema eti ananipenda. Wakati huu, labda unafikiria, "Hili ni jambo la kushangaza," ama, "Kwa nini alikuwa mjinga hivi," lakini muda huu wote, nimekuwa haswa nikiongea juu yako. Nakuhakikishia kuna watu kadhaa wanaonisikiliza saa hii ambao wananyanyaswa au ambao walinyanyaswa wakiwa watoto au walio wanyanyasaji wenyewe. unyanyasaji unaweza kuwa unamwathiri binti yako, dadako, rafiki yako wa karibu wakati huu. Niliweza kumaliza hadithi yangu wazimu ya mapenzi kwa kuvunja ukimya. Bado naendelea kuvunja ukimya leo. Ni njia yangu ya kusaidia waathirika wengine, na ni ombi langu la mwisho kwenu. Ongeeni kuhusu mliyosikia hapa. Unyanyasaji hushamiri tu katika ukimya. Una nguvu ya kumaliza unyanyasaji majumbani kwa kuongea kuhusu unyanyasaji. Sisi waathirika tunahitaji kila mtu. Tunawahitaji nyote kuelewa siri za unyanyasaji majumbani. Mulikieni mwanga unyanyasaji kwa kuuongelea mkiwa na watoto wenu, wafanyakazi wenzenu, marafiki zenu na familia. Ongeleeni waliosalimika kama watu wema na wanaopendeka walio na maisha kamili kwenye siku za usoni Eleweni ishara za mapema za tuhuma na muingilie kati kistadi malizeni na muonyeshe waathirika njia safi ya kuiepuka. Pamoja tunaweza kufanya vitanda vyetu, meza zetu za mlo na familia zetu mahali pa amani zinavyopaswa kuwa Asanteni. (Mahali)